Jumatano , 27th Jan , 2016

Imeelezwa kuwa kati ya wanawake 6000 waliopimwa katika mikoa nane ya Tanzania, wanawake 2000 walibainika kuwa na dalili za saratani ya shingo ya kizazi.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto nchini Tanzania imesema kuchelewa kugundulika kwa saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake nchini kumechangia wanawake wengi kufariki dunia kwa saratani hiyo kutokana na kufika kupata matibabu wakati wakiwa wamechelewa.

Saratani ya Shingo ya kizazi inatajwa kuwa ni saratani ya nne inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake katika nchi zinazoendelea.

Ripoti ya mwaka 2012 ya shirika la afya duniani ‘WHO’ imesema kuwa, kati ya matukio 75,000 ya waathirika wa saratani ya kizazi barani Afrika, 50,000 walifariki dunia huku Tanzania ikiwa na kiwango kikubwa cha vifo vitokanavyo na saratani hiyo katika nchi za Afrika Mashariki sababu kubwa ikiwa ni wanawake kuchelewa kugundua dalili za saratani hiyo mapema.

Mkurugenzi Mtendaji wa chama cha Chama cha Uzazi na Malezi Bora Tanzania (UMATI), Lulu Ng'wanakilala amesema uchache wa wataalamu ni changamoto kubwa nchini.

Kwa upande wake Dkt. Mashafi Joseph Mashafi kutoka shirika lisilo la kiserikali la PSI-Tanzania, amesema kati ya wanawake 6000 waliopimwa katika mikoa nane ya Tanzania wanawake 2000 walibainika kuwa na dalili za saratani hiyo licha ya changamoto ya uchache wa wataalam.