Jumatatu , 30th Nov , 2015

Watanzania wametakiwa kuwapeleka watoto wao katika vyuo mbalimbali vya ufundi stadi kwa kuwa ndio elimu inayozalisha ajira nyingi kuliko vyuo vikuu hapa nchini ili kuepukana na tatizo la ajira.

Mwenyekiti wa bodi ya vyuo vya Veta nyanda za juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Ruvuma na Njombe,Bw, Kabaka Ndenda

Inadaiwa kuwa watu wanaojiajiri wengi wanatoka katika vyuo vya ufundi kuliko wanaomaliza vyuo vikuu kwa kuwa wahitmu wengi wa vyuo vikuu wanategenea kuajiriwa huku wa vyuo vya ufundi wakijikita kujitengenezea ajira kwa kujiajiri wenyewe.

Kauli hiyo imetolewa na mwenyekiti wa bodi ya vyuo vya Veta Nyanda za Juu Kusini inayojumuisha mikoa ya Iringa, Ruvuma na Njombe Bw, Kabaka Ndenda, katika mahafari ya kwanza ya chuo cha Veta Wilaya ya Makete na kuongeza kuwa kuwa vijana wengi wanaomaliza katika vyuo vya ufundi wanauhakika wa ajira kuliko wanaohitimu vyuo vikuu.

Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Ramadhani Sebo amesema wanafunzi hao wanaenda kuajirika licha ya kuwa na changamoto za vifaa vya kufundishia katika baadhi ya fani zinazofundishwa katika chuo hicho.

Aidha ameongeza kuwa chuo hicho kilianza na kozi mbili na sasa kina kozi 4 huku kikifundisha masomo mtambuka ambayo yanatoa nafasi za ajira kwa haraka zaidi.

Kwa upande wako Wanafunzi wanaosoma katika chuo hicho wameiomba serikali kuongeza uwezeshwaji kwa vijana wanaojiajiri.