Ijumaa , 19th Mei , 2023

Serikali Kanda ya Ziwa imesema haitawafumbia macho watendaji wa sekta ya afya wanaokwamisha jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maboresho sekta ya afya.

Baadhi ya watumishi wa sekta ya afya kanda ya ziwa

Akizungumza katika kikao kazi cha watendaji hao wa Kanda ya Ziwa kwa mikoa mitano ya Mwanza,  Simiyu, Mara Geita na Shinyanga na Bohari ya Dawa (MSD), Katibu Tawala wa Mara Msalika Makungu, amesema lengo la Rais Dk.Samia kufanya maboresho ya sekta hiyo ni kumpatia huduma bora mwananchi.

"Ni muhimu wataalamu watimize majukumu yao kwa weledi na huduma ziwafikie wananchi kwa kuwa sekta ya afya ni sekta mtambuka yenye tija katika utekelezaji wa malengo ya mpango wa serikali kijamii na kiuchumi," amesema 

Kwa upnde wake Meneja wa Kanda hiyo wa MSD, Egidius Rwezaura, alisema hivi karibuni wanatarajia kupokea vifaa vya afya zikiwemo dawa na vifaa tiba aina 100 ikiwemo vitanda na mshine za maabara ambavyo vitamaliza changamoto ya mahitaji yaliyopo.

Naye Mfamasia Mratibu Kiongozi wa Huduma za Bidhaa za Afya kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mathew Mganga, alisema watendaaji hao watambue kuwa Rais ametoa fedha nyingi za dawa na vifaa ni vyema zitumike katika ununuzi wa bidhaa hizo na sio matumizii mengine.

Alisema lengo la maboresho sekta hiyo, ni kufanikisha huduma bora kwa wananchi ambapo bado fedha zinazomiminika na hatua zilizochukuliwa na serikali ya Rais Dk.Samia haiendani na huduma bora wanazopatiwa wananchi hivyo ni lazima kuchukua hatua.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk.Zabron Masatu, alisema wamepokea maelekezo hayo wataenda kubanana ndani katika utendaji kuweza kufikia lengo la Rais katika maboresho ya huduma bora za afya kwa wananchi.