Jumatatu , 24th Sep , 2018

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), imebainisha kuwa zaidi ya waombaji wa mikopo ya elimu ya juu 25,000 kwaajili ya mwaka wa masomo 2018/2019, wana changamoto kwenye fomu zao za maombi.

Makao makuu ya bodi ya mikopo.

Kupitia taarifa yake HESLB, imefafanua kuwa imepokea jumla ya maombi 78,833 lakini kati yao zaidi ya 25,000 wana makosa mbalimbali ikiwemo kutowasilisha vithibitisho vya sifa ya mtu anayestahili kupata mkopo.

''Baada ya kukamilika kwa muda wa kupokea maombi ya mikopo Julai 31, 2018, HESLB,  imepokea jumla ya maombi 78,833, na baada ya uhakiki, tumebaini waombaji zaidi ya 25,000 fomu zao zina upungufu wa nyaraka na uthibitisho wa kuwezesha kuendelea na hatua inayofuata ya kupangiwa mikopo katikati ya mwezi Oktoba, 2018'' imeeleza taarifa hiyo.

Aidha HESLB imetoa muda wa siku 7 yaani wiki moja kwa waombaji hao kupitia upya fomu zao na kufanya marekebisho kwa njia ya mtandao. Zoezi hilo linaanza leo Jumatatu  Septemba 24 hadi Jumapili  Septemba 30, 2018.

Mbali na hayo bodi ya mikopo pia imewatahadharisha waombaji wa mikopo dhidi ya matapeli wanaolaghai watu kuwa wanaweza kuwasaidia kupata mikopo.