
Wanajeshi wa jeshi la anga nchini Nepal wakiendelea na shughuli za kuopoa miili ya wahanga wa ajali
Video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii inaonesha ndege ikiruka chini kwenye eneo lenye watu wengi kabla ya kupata adha hiyo. Kulikuwa na abiria 68 ndani ya ndege hiyo, wakiwemo angalau raia 15 wa kigeni, na wafanyakazi wanne.
Wanajeshi 200 wa Nepal wanahusika katika uokoaji katika eneo la ajali kwenye korongo la Mto Seti, kilomita moja na nusu tu kutoka uwanja wa ndege. Video ya eneo la ajali inaonesha moshi mnene unaofuka na uchafu unaowaka.
Waziri Mkuu Pushpa Kamal Dahal ameitisha kikao cha dharura cha baraza lake la mawaziri na kuvitaka vyombo vya dola kufanyia kazi shughuli za uokoaji.
Kati ya abiria hao, 53 wanasemekana kuwa Wanepali. Kulikuwa na Wahindi watano, Warusi wanne na Wakorea wawili kwenye ndege. Pia kulikuwa na abiria mmoja kutoka Ireland, Australia, Argentina na Ufaransa miongoni mwa wengine.