Alhamisi , 20th Oct , 2022

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka watumishi wa umma watimize wajibu wao kama ambavyo Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia wafanye pindi anapowateua ama kuwapa ajira.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,

Ametoa wito huo wakati akizungumza na viongozi wa mkoa, wilaya na watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Madaba kwenye ukumbi wao mara baada ya kuzindua jengo la Halmashauri hiyo. 

"Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, anataka kuona watumishi wa umma mkiwatumikia Watanzania, nenda kwa wananchi mkawasikilize, huwezi kuwahudumia bila kuwasikiliza na huwezi kujua changamoto zao bila kuwasikiliza," amesema Waziri  

 Amewataka viongozi na watumishi hao wafanye kazi kwa kulenga matokeo. "Nataka tufanye kazi kwa matokeo, tufuate maelekezo na tuzingatie nidhamu, tuna fedha za ndani na za serikali kuu, tuzisimamie vizuri na naomba msijiingize kwenye matumizi mabaya ya fedha hizo,"

Waziri Mkuu aliwapa mfano wa Mkuu wa shule ya sekondari Irugwa ambaye alipokea shilingi milioni 120 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa sita, lakini alizisimamia vizuri akamaliza madarasa, akajenga matundu matano ya vyoo, kuweka mfumo wa maji ya mvua na chenji iliyobakia akapiga lipu mabweni ya wasichana na kujenga mabafu licha ya kuwa shule iko kisiwani na kisiwa kiko mbali kutoka Nansio na pia kiko mbali kutoka Mwanza ambako mahitaji yote yanafuatwa. 

Naye, Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama, alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia wana Madaba shilingi bilioni 14.2 ambazo zimetumika kujenga miradi ya maji, barabara za vijijini, miundombinu ya afya na elimu.