Wawili mbaroni kufuatia kifo cha mwana CCM Iringa

Jumatatu , 28th Sep , 2020

Mkuu wa mkoa wa Njombe, Mhandisi Marwa Rubirya, amesema kuwa tayari watuhumiwa 2, wanashikiliwa na jeshi la polisi kufutia kifo cha aliyekuwa Mwenyekiti wa UVCCM vyuo na vyuo vikuu mkoa wa Iringa aliyeuawa kikatili Septemba 20 na mwili wake kutupwa na watu wasiojulikana.

Kushoto ni Dkt. Frank Hawasi akikabidhi fedha za rambirambi zilizotolewa na Rais Magufuli kwa mzee Polkap Mlelwa, Baba mzazi wa marehemu Emmanuel Mlelwa

Mhandisi Rubirya, ameitoa kauli hiyo wakati wa mazishi ya kijana huyo, Emmanuel Mlelwa, yaliyofanyika katika kijiji cha Luvuyo kilichopo Kata ya Madope wilayani Ludewa.

Aidha kufuatia msiba huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli, ametoa salamu za pole na ubani wa shilingi milioni 5 kwa familia ya mzee Polkap Mlelwa, kufuatia kifo cha kijana wake, fedha ambazo ziliwasilishwa na Dkt. Frank Hawasi ambaye ni katibu wa NEC uchumi na fedha wa CCM Taifa.

Kijana Emmanuel Polkap Mlelwa aliyekuwa mwanafunzi wa chuo kikuu cha Iringa alikuwa mkoani Njombe kwa ajili ya likizo na alitoweka tangu Septemba 20.