Wahamiaji hao wa kusini mwa jangwa la Sahara walikuwa wakijaribu kuvuka bahari ya Mediterania kuingia Italia.
Ni tukio la hivi karibuni katika msururu wa mashua ya wahamiaji kuzama katika pwani ya Tunisia katika siku chache zilizopita, huku nyingine tano zikizama katika kipindi cha siku nne zilizopita.
Hii ni baada ya Tunisia kuanzisha kampeni dhidi ya wahamiaji wa Kiafrika wasio na vibali.Wakati huo huo, maafisa wa Italia katika kisiwa cha Lampedusa wanasema wamezidiwa nguvu, baada ya rekodi ya wahamiaji 2,500 kuwasili katika muda wa saa 24 zilizopita.
Waziri Mkuu wa siasa kali za mrengo wa kulia nchini Italia, Giorgia Meloni, ameionya Ulaya hatari ya kushuhudia wimbi kubwa la wakimbizi wanaowasili katika mwambao wake.
Tunisia imekuwa kitovu cha wahamiaji wanaotaka kuingia Ulaya, huku takwimu za Umoja wa Mataifa zikionyesha wahamiaji wasiopungua 12,000 waliotua katika fukwe za Italia mwaka huu wakiachwa kutoka Tunisia. Idadi hiyo ilikuwa 1,300 tu katika kipindi kama hicho mwaka jana.





