Jumatatu , 9th Jun , 2014

Kampuni inayotafiti mafuta na gesi nchini Tanzania ya Swala Oil and Gas, leo imetangaza kuanza kuuza hisa zake ili kila Mtanzania awe sehemu ya umiliki wa rasilimali za mafuta na gesi.

Mkurugenzi wa kampuni ya Swala Oil and Gas, Abdullah Mwinyi (kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na mbunge wa bunge la Afrika Mashariki kutoka Tanzania Bi. Shyrose Bhanji.

Kampuni hiyo inatafuta mafuta kwenye kitalu kijulikanacho kama Kilombero kilichopo mkoani Morogoro na kitalu cha Pangani kinachopatikana kaskazini mashariki mwa Tanzania, ambapo afisa mtendaji mkuu wake Bw. David Mestres Ridge amesema maeneo yote hayo yameonesha dalili nzuri za uwezekano wa kupatikana kwa mafuta na gesi.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw. Abdullah Mwinyi, amesema hatua ya kampuni hiyo kutangaza kuuza hisa zake ni ya kwanza kufanywa na kampuni zinazotafuta mafuta na gesi nchini ambapo kila mtanzania ataruhusiwa kununua hisa zisizozidi mia moja ili kutoa fursa kwa idadi kubwa ya watu.

Mwinyi ameongeza kuwa mbali ya kuuza hisa, kampuni hiyo pia imetenga asilimia tisa kati ya asilimia 35 ya hisa inazomiliki kutoka katika kampuni mama ya Swala Energy ya nchini Australia, na kuzigawa hisa hizo kwa wakazi wa vijiji ambako kampuni hiyo inatafuta mafuta na gesi.

Uamuzi huo wa Swala Oil and Gas Tanzania Ltd, unaunga mkono wito wa taasisi ya sekta binafsi nchini TPSF, ambayo imekuwa ikitaka kuwepo kwa ushiriki mpana wa Watanzania wazawa, hususani katika usimamizi, uendeshaji na ushiriki katika uchumi wa mafuta na gesi, ikiwa ni pamoja na kuandaliwa kwa mazingira mazuri ambayo yatawezesha ushiriki wa wazawa.