Jumapili , 23rd Nov , 2025

Mwili wa marehemu umeonekana jana Novemba,22 2025 majira ya saa 01:30 asubuhi katika fukwe ya bahari ya Hindi kwenye miti ya mikoko mtaa Mangoela ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake pamoja na kuwekewa mchanga wenye tope mdomoni na puani.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mtwara limeanza kufanya uchunguzi wa tukio la mauaji ya Sumaya Hassan Mataka, mwenye umri wa miaka kumi na mbili (12) mwanafunzi wa darasa la tano katika shule ya msingi Ufukoni, mkazi wa mtaa wa Ufukoni stendi ambaye mwili wake umekutwa katika fukwe ya bahari ya Hindi katika Wilaya ya Mtwara.

Imeelezwa kuwa marehemu alitoka nyumbani kwao tarehe 21 Novemba, 2025 majira ya asubuhi akiwa na watoto wenzake na kuelekea maeneo ya mangoela na baada ya hapo hakurudi tena nyumbani.Jitahada za kumtafuta marehemu zilifanyika ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa katika kituo cha Polisi Kati Mtwara juu ya kutoweka kwake.

Mwili wa marehemu umeonekana jana Novemba,22 2025 majira ya saa 01:30 asubuhi katika fukwe ya bahari ya Hindi kwenye miti ya mikoko mtaa Mangoela ukiwa na majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake pamoja na kuwekewa mchanga wenye tope mdomoni na puani.

Uchunguzi wa awali umebaini kwamba kifo cha marehemu kimetokana na kukosa hewa baada ya kuwekewa mchanga wenye tope mdomoni na puani wakati akifanyiwa vitendo vya ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa kijinsia. Mwili wa Marehemu umekabidhiwa kwa ndugu kwaajili ya taratibu za mazishi.

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa yeyote mwenye taaarifa za kweli na uhakika kuhusiana na tukio hili asisite kuziwasilisha kwa Polisi au mamlaka yoyote atakayoona inafaa ili isaidie kuwakamata waliohusika na tukio hili la kikatili.