Jumatatu , 15th Jan , 2018

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema baadhi ya Madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili wanatakiwa kuhamia Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo alipotembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke ili kuangalia hali ya utoaji wa huduma za afya kwa wananchi hospitalini hapo, ambapo amesema lengo ni kuongeza rasilimali watu kwa ajili ya kumudu hali ya ongezeko la wagonjwa wanaohitaji.

"Kubwa nililoligundua hapa ni kuna mlundikano wa idadi kubwa ya wanaohitaji huduma hivyo wale madaktari tunaowatoa Muhimbili hasa madaktari bingwa baadhi tutawahamishia hapa ili kusaidiana na madaktari wa Temeke katika kutoa huduma bora kwa watu wengi zaidi" alisema Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy amesema kuwa Serikali ipo mbioni kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya kujenga jengo la ghorofa nne mapema mwaka huu, ambalo litachangia katika kuondoa tatizo la mlundikano wa wagonjwa hospitalini hapo.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Temeke Dkt. Amani Malima amesema kuwa wapo mbioni kuagiza vifaa na vifaa tiba pamoja na kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wengi zaidi.