Jumatatu , 4th Jan , 2021

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki, amewataka wakurugenzi wa halmashauri zenye masoko ya samaki ya kimataifa kuacha kupanga tozo za mazao ya uvuvi bila kuwasiliana na wizara hiyo ili kuondoa kero za tozo zinazowakumba wananchi wanaofanya biashara katika maeneo hayo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki

Hayo ameyabainisha mara baada ya kutembelea mnada wa mifugo uliopo Kijiji cha Buzirayombo, Kata ya Bukome na soko la samaki la kimataifa lililopo Kijiji cha Kasenda Kata ya Muganza, wilaya ya Chato mkoani Geita, Waziri Ndaki amesema wizara haitaki kusikia kero za wafanyabiashara kuhusu tozo zisizo rafiki katika masoko hayo.

"Kuhusiana na tozo niseme tu kwa wakurugenzi walio na masoko haya ya kimataifa kwa maana ya soko la Kirumba na Kasenda, sisi Wizara hatutaki kusikia kelele katika haya masoko mnapopanga tozo zenu hakikisheni kwa masoko haya mawili tuwasiliane ili tupange tozo za kwenu na kwetu ambazo zitakuwa rafiki", amesema Waziri Ndaki.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chato Dkt. Medard Kalemani, amemuomba Waziri Ndaki kupitia vikundi vya wavuvi vilivyosajiliwa, wizara ione namna ya kuwasaidia wavuvi mikopo yenye riba nafuu pamoja na kuwanunulia nyavu ili kuacha kujihusha na uvuvi usiofuata utaratibu.