
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katika taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari leo, ametoa ufafanuzi huo na kukanusha taarifa za kuwepo kwa ugonjwa huo, huku akirejea kauli yake kuhusu ugonjwa huo aliyoitoa mwezi Februari mwaka huu kuwa ugonjwa huo haujaingia nchini.
Kuhusu utafiti uliofanywa na Taasisi ya NIMR, amesema kuwa utafiti huo ulifanyika nchini kuchunguza ubora wa kipimo kipya cha kupima magonjwa ya zika na chikungunya.
Amesema kwa utaratibu wa kitafiti, hiyo ni hatua ya awali ya kuangalia ubora na uwezo wa kipimo hicho na kwamba matokeo yake bado yanahitaji kuchunguzwa kwa kina kupitia vipimo vilivyothibitishwa na Shirika la Afya Duniani.
Taarifa hiyo imesema kuwa wizara kwa kushirikiana na taasisi na ndani na nje ya nchi inaendelea na utafiti na ufuatiliaji wa kitaalamu ili kuzuia ugonjwa huo kuingia nchini na tayari imeshaandaa mkakati wa zika ambao unaelekeza utekelezaji wa ufuatiliaji wa zika.
Dkt. Mwele Malecela akizungumza na wanahabari jana (Desemba 15, 2016)
Kwa mujibu wa Utafiti ulifanywa na Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini, (NIMR) iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kupitia mkurugenzi wake Dkt. Mwele Malecela ilisema kuwa Tanzania ina wagonjwa wa zika ambapo asilimia 15.6 ya watu waliopimwa kati ya mwaka 2015 na 2016 walibainika kuwa na virusi vya ugonjwa huo.