Waziri atakiwa kuachia ngazi

Jumatano , 15th Mei , 2019

Mbunge wa Moshi Vijijini Anthony Komu amependekeza Wabunge kufikia maamuzi ya kumtaka Waziri wa Mambo ya Nje Prof Palamagamba Kabudi kuwajibika, kwa kile alichokidai kuna baadhi ya mambo ambayo amekuwa akiyashauri hayaendi sawa.

Waziri wa Mambo ya Nje Prof Palamagamba Kabudi.

Mbunge Komu ametoa kauli hiyo Bungeni Jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ambapo amesema Profesa Kabudi anashauri mambo yasiyokuwa na manufaa.

"Sakata la korosho upinzani tumesema watu wawajibike,  tuliingia mkataba kampuni ya Kenya na Waziri Kabudi alikuwepo akasema kampuni hiyo ina uzoefu, lakini baada ya miezi 4 imeonekana haina uwezo, kweli Bunge hili linakubali Kabudi aendelee na Uwaziri wake?" amesema Komu.

Akichangia kwenye mjadala huo, Mbunge Tandahimba, Katani S Katani amesema, "wamempotosha sana Rais kwa sisi waislam Kangomba sio dhambi, ipo hadithi inayosema sio haramu, Waziri wa Biashara yupo hapa watu hawajapata fedha mpaka leo, wapo waliopata fedha mwezi 4 mtu anadai Mil. 59, anaingiziwa Mil. 9 anadai ziolizobaki, mimi nadai milioni 48 nimeingiziwa Mil 8 nyingine naendelea kudai".

Kwa sasa Bunge linaendelea jijini Dodoma ambapo Mawaziri mbalimbali wameendelea kuwasilisha Makadirio yao ya bajeti kwa mwaka fedha 2019/2020.