Ijumaa , 23rd Nov , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa vyuo vikuu vyote nchini, vya binafsi na vya umma ili viendelee kutoa elimu ya juu yenye ubora na viwango vinavyotakiwa kwa lengo la kukidhi matakwa na ushindani kwenye soko la kitaifa na kimataifa.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Amesema suala hilo ni muhimu likapewa uzito unaostahili kwani wahitimu hao wakitoka vyuoni wanakwenda kutoa huduma katika jamii ya watanzania na pia ya kimataifa, hivyo ni muhimu elimu inayotolewa ikazingatia ubora na viwango vinavyostahiki.

Amesema Serikali ya awamu ya tano, inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi hususani wa vyuo vikuu binafsi kama Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana cha Tanzania, katika maendeleo ya elimu ya juu.

Serikali inatambua mchango wa vyuo hivyo katika kupanua fursa kwa Watanzania wengi kupata elimu ya juu, ambapo hadi sasa udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwenye vyuo vikuu binafsi nchini ni takriban asilimia 25 ya wanafunzi wote.”

Waziri Mkuu amesema baadhi ya wahitimu watapata ajira lakini si kila mhitimu atapata fursa ya kuajiriwa, hivyo Serikali itaendelea kuunga mkono azma yao kama chuo kikuu ya kutoa wahitimu wenye tabia, utashi na uwezo wa kutengeneza kazi na siyo watafuta kazi tu.