Jumamosi , 24th Mar , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amekagua ukarabati wa kituo cha afya cha Kata ya Mbekenyera na kuwaeleza wananchi hao kuwa dhamira ya serikali ni kuwahudumia wananchi wote kiujumla katika kupata huduma zilizokuwa bora.

Waziri Mkuu ambaye yuko wilayani Ruangwa kwa ziara ya kikazi ya siku mbili amesema serikali imetoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi ya kujifungulia, maabara, wodi ya wanawake na wanaume na chumba cha upasuaji.

"Serikali imeamua kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga na kuboresha vituo vya afya ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma za afya karibu na makazi yao", amesema Waziri Majaliwa.

Aidha, Waziri Mkuu amewataka wananchi hao waendelee kuiunga mkono serikali yao, ambayo imedhamiria kuwatumikia ili waweze kupata maendeleo.

Pia, Waziri Mkuu amekabidhi gari la kubeba wagonjwa katika kituo hicho. Gari hilo limetolewa na Rais Dkt. John Magufuli ili kuimarisha huduma za afya kituoni hapo.