Jumapili , 22nd Sep , 2019

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameitaka Mamlaka ya Usajili wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ihakikishe wananchi hasa walioko vijijini wanapata angalau namba za utambulisho wa usajili wao, kabla ya muda wa usajili wa laini za simu haujamalizika.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika katika Uwanja wa Hospitali ya Wilaya ya Geita,  iliyopo kwenye Kijiji cha Nzela.

Amesema kitendo cha kuwapatia namba za utambulisho wa usajili wananchi ambao hawajapata vitambulisho vya uraia kitawezesha kuingia kwenye orodha ya wale wanosubiri kusajiliwa, hata kama muda wa usajili utakuwa umeisha.

"NIDA mnalalamikiwa, nimeenda Morogoro Vijijini NIDA mnalalamikiwa hivi utendaji wenu uko je? Kwanini mnachelewa, naomba muondoe haya malalamiko kwa ya wanachi kabla ya zoezi la usajili wa laini za kieltroniki liishe." amesema Waziri Mkuu

Aidha Waziri Mkuu aliwasihi wananchi wote kuwa walinzi wa nchi yao kwa kutoa taarifa za watu ambao wanaomba vitambulisho vya uraia wa Tanzania wakati si raia.