
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi wakati alipowasili kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma kuzindua Mradi wa USAID AFYA YANGU Mei 6, 2022. Wengine kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, Balozi wa Marekani nchini Dkt. Donald Wright na kulia ni Mkurugenzi Mkazi wa USAID, Kate Somvongsiri
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Mei 6, 2022) wakati akizindua mradi wa USAID Afya Yangu ama Comprehensive Client Centered Health Program (C3HP) unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Watu wa Marekani (USAID Tanzania).
“Mamlaka za Serikali za Mitaa toeni ushirikiano wote utakaofanikisha utekelezaji wa mradi huu kwa mafanikio. Watendaji wabadhirifu wasipewe nafasi kuhujumu mradi huu. Viongozi, fuatilieni mara kwa mara ili kuhakikisha malengo ya mradi yanatekelezwa na kuleta tija.”
Amesema azma ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora za afya, hivyo imeendelea kuweka kipaumbele katika sekta ya afya kwa kutekeleza mikakati ya kuimarisha utoaji wa huduma. “Mojawapo ya vipaumbele ni mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI.”
Waziri Mkuu amesema kuwa jitihada mbalimbali za Serikali pamoja na wadau zimeanza kuzaa matunda, ambapo katika kutekeleza mkakati wa kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kwa kiasi kikubwa kiwango cha maambukizi kimeshuka kutoka asilimia 13.5 mwaka 2015 hadi asilimia saba mwaka 2020.
Majaliwa amesema Serikali imeweka kipaumbele katika kupambana na vifo vinavyotokana na uzazi na watoto wachanga kwa kutekeleza Mpango wa Kuimarisha Afya ya Msingi. “Mpango huu ulitutaka kuongeza vituo vya afya ili kila kata iwe na kituo cha afya.”
“Hadi kufikia mwaka 2020 jumla ya vituo vya afya 487 na hospitali za wilaya 102 zimejengwa au kukarabatiwa ili kutoa huduma za afya ya msingi ikiwemo ya upasuaji wa kumtoa mtoto tumboni, haya ni mafanikio makubwa sana.”
Amesema ongezeko la vituo hivyo linaifanya Tanzania kuwa kati ya nchi zilizo chini ya Jangwa la Sahara ambazo zimefikia kwa kiasi kikubwa vigezo vya Umoja wa Mataifa vya Utoaji Huduma za Dharura za Uzazi na Mtoto Mchanga.
Ametaja vigezo hivyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za dharura kwa kuzingatia idadi ya watu na jiografia ya maeneo, kiwango kikubwa cha akinamama wanaojifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma na kiwango cha kuridhisha cha wajawazito.
Akizungumzia kuhusu mradi wa USAID Afya Yangu amesema amefurahishwa sana na mradi huo ambao una nia ya kuongeza upatikanaji na matumizi ya huduma ya afya ya uzazi hapa nchini ambao unalenga kumuwezesha mtu binafsi aweze kuimarisha uwezo wake wa kuwa na tabia chanya katika kuzingatia mahitaji ya afya yake.
Malengo mengine ni kumuwezesha mtu kujihudumia mwenyewe pamoja na upatikanaji wa huduma ya afya ya uzazi na mtoto kwa mtu binafsi. Pia, umelenga kuweka mazingira wezeshi ya utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi na mtoto.