Alhamisi , 23rd Mei , 2019

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imeanza jitihada za kufuta tozo zote ambazo zinakwamisha mazingira ya ufanyaji wa biashara nchini zikiwemo za pembejeo ili kuwawezesha wafanyabiashara kuzifikisha hadi ngazi ya kijiji kwa wakulima. 

Waziri Majaliwa.

Ametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2019 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la mbunge wa Madaba, Kizito Mhagama katika kipindi cha maswali kwa Waziri Mkuu. Mbunge huyo alitaka kujua serikali ina mpango gani wa kupunguza tozo kwa maduka yanayouza pembejeo ili kumwezesha mkulima kupata pembejeo.

Waziri Mkuu amesema serikali imepokea malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo na wauzaji wa pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima za biashara zao.

Serikali imesikia vilio vyenu na sasa inafanya mapitio ya tozo hizo na itakapofikia hatua nzuri itawajulisha na kuwashirikisha kujua ni aina gani ya tozo ambayo itaondolewa au kuibadilisha ili muendelee kufanya biashara zenu katika mazingira rahisi", amesema Majaliwa. 

Waziri Mkuu amesema kazi kubwa inayofanywa na serikali kwa sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote kuanzia kwa wakulima hadi kwa wafanyabiashara na kutengeneza mazingira mazuri ya kufanya biashara nchini, ikiwemo ya pembejeo ili kuzifikisha kiurahisi kwa wakulima.