Jumatatu , 6th Oct , 2025

Waziri Mkuu wa Ufaransa Sébastien Lecornu amejiuzulu, chini ya siku moja baada ya baraza lake la mawaziri kutangazwa.

Ikulu ya Elysée ilitoa tangazo hilo baada ya Lecornu kukutana na Rais Emmanuel Macron kwa saa moja Jumatatu asubuhi.

Hatua hiyo ya kushangaza inajiri siku 26 baada ya Lecornu kuteuliwa kuwa waziri mkuu kufuatia kusambaratika kwa serikali ya awali ya François Bayrou.

Vyama vyote katika Bunge la Kitaifa vilikosoa vikali muundo wa baraza la mawaziri la Lecornu, ambalo kwa kiasi kikubwa halijabadilishwa kutoka la Bayrou, na kutishia kupiga kura kulisambaratisha.

Vyama vingi sasa vinataka uchaguzi wa mapema, huku baadhi wakimtaka Macron ajiuzulu - ingawa amekuwa akisema hatajiuzulu kabla ya muhula wake kumalizika 2027.

"Jambo la busara la kufanya sasa ni kufanya uchaguzi," amesema Marine Le Pen wa chama cha mrengo wa kulia, National Rally (RN).

Lecornu - waziri wa zamani wa majeshi na mtu wa karibukwa Macron - alikuwa waziri mkuu wa tano wa Ufaransa katika kipindi cha chini ya miaka miwili.

Siasa za Ufaransa zimekuwa na msukosuko mkubwa tangu Julai 2024, wakati uchaguzi wa bunge uliposababisha kokosekana chama chenye wingi wa viti.

Hii imefanya kuwa vigumu kwa waziri mkuu yeyote kupata uungwaji mkono unaohitajika kupitisha miswada yoyote.
Serikali ya Bayrou ilipigiwa kura ya kutokuwa na imani mwezi Septemba baada ya bunge la Ufaransa kukataa kuunga mkono bajeti yake ya kubana matumizi, ambayo ililenga kupunguza matumizi ya serikali kwa €44bn ($51bn; £38bn).