Alhamisi , 4th Mar , 2021

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema ameridhishwa na kazi kubwa ya kupambana na makundi ya Nzige yaliyovamia nchini iliyofanywa na Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana mashirika mawili ya kupambana na Nzige barani Afrika.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangaliwa Nzige walioangamizwa katika kijiji cha Engaruka Monduli

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Machi 4, 2021, wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Engaruka, wilayani Monduli mkoani Arusha mara baada ya kukagua shughuli ya udhibiti wa Nzige katika kata ya Engaruka.

"Lazima tuwateketeze, Nzige ni hatari na hawapaswi kupewa nafasi hata ya dakika moja kuingia kwenye mashamba yetu hawa wana uwezo wa kusafiri umbali wa kilomita 200 kwa siku na kuteketeza zaidi ya hekta mbili kwa siku, hivyo ni lazima tuwateketeze," amesema Waziri Mkuu.

 “Muhimu zaidi ni kujipanga vizuri kukabiliana nao ni lazima tuendeleze kazi nzuri tuliyoianza, hawa wadudu ni hatari na wanazaliana mno, ukimuona kawaida anakuwa na rangi nyekundu lakini ukimuona ana rangi ya njano huyo amebeba mayai tuwatekeze ili wasizaliane," ameongeza Waziri Mkuu. 

Waziri Mkuu amesema watalaamu wa Tanzania na wataalamu kutoka Zambia, Zimbabwe, Uganda na Kenya wanashirikiana kupambana na Nzige kwa kutumia vifaa mbalimbali kama ndege, helikopta na mitambo ya kupulizia kwa mikono.