Jumanne , 2nd Sep , 2025

Kuelekea kilele cha maadhimisho kuwakumbuka mashujaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Septemba 7 mwaka huu, Mwenyekiti wa CHADEMA kanda ya Victoria Ezekiah Wenje, amesema watu wote ambao bado wapo ndani ya chama hicho ni mashujaa.

Ametoa kauli hiyo wakati akichangia kwa njia ya mtandao na Baraza la Kidigitali la chama hicho leo Septemba 2, na kuongeza kuwa tangu chama hicho kianzishwe kimepata madhila mengi yaliyofanya wengine kuhama , wengine kuwa walemavu na hata kupoteza maisha.

“Haya yaliyookea kwetu yanatokea nchi mbalimbali. Lakini kuna faraja kwa sababu hadi viongozi wa dini wanapinga mambo haya, watu wanaona ni faraja kwetu.”

Ameongeza kuwa serikali yoyote inayotumia nguvu nyingi kubaki madarakani iko mbioni kuanguka na kuwataka wanachama wa chama hicho kutokata tamaa.

“Kila familia ina kovu, hata mimi kuna kaka yangu aliuawa. Tufarijiane tusikate tamaa. Tukikata tamaa tutakuwa tunawasaliti wenzetu waliotangulia kama kina Alphonce Mawazo na Mdude walioacha watoto wadogo” ameongeza.