Jumapili , 2nd Feb , 2020

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, imesema kuwa hadi leo Februari 2,2020 haijapokea waraka wowote unaotoa taarifa za kumzuia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwenda nchini Marekani kama ambavyo taarifa zinasambaa mitandaoni.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Akizungumza na EATV&EA Radio Digital, Mkurugenzi wa Mawasiliano kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Emmanuel Buhohela, amesema kuwa Serikali ya Tanzania huwa haijishughulishi na masuala ya mitandaoni hivyo bado wanangoja taarifa rasmi.

"Hatuna taarifa yoyote mpaka sasa hivi kwahiyo tutakapozipata tutazitoa, Serikali inazungumza kwa documents kwahiyo hatuwezi kusikia taarifa za kwenye mitandao na sisi tukazijibu" amesema Buhohela.

Januari 31, 2020, kupitia ukurasa wa Twitter wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Michael Pompeo, aliandika kuwa wamemzuia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, kuingia nchini humo, kutokana na tuhuma za kujihusisha na vitendo vinavyokiuka haki za binadamu.