Ijumaa , 20th Jan , 2023

Chama cha Mapinduzi (CCM), kimetoa wiki moja kwa Wizara ya Elimu kuanzia leo Januari 20, 2023, kuhakikisha vishikwambi vilivyotolewa na serika kwa ajili ya walimu vinawafikia walengwa. 

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Sophia Mjema,

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Sophia Mjema, amesema kwamba chama hicho kimepokea malalamiko ya kutotekelezwa kikamilifu kwa maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuhusu ugawaji wa vishikwambi hivyo.

"Ulitengwa muda maalumu wa kutolewa kwa vishikwambi hivi ambao ulikuwa unaishia Januari 15, mwaka huu, lakini chama kimepokea malalamiko kwamba hadi leo kuna baadhi ya makundi hayajapata hivyo vishikwambi. Lakini pia kuna baadhi ya wilaya hawajagawa kabisa vishikwambi hivyo," amesema Sophia Mjema

Aidha Mjema ameongeza kuwa, "Chama kinatoa maelekezo, kinaielekeza Wizara husika (Wizara ya Elimu) kuhakikisha zoezi hili linakamilika na walengwa wote wanaostahili kuhakikisha wamepata vishikwambi hivyo, lakini so hivyo tu bali pia wahakikishe malalamiko haya hayapo na wasimamie zoezi kuona makundi yaliyopaswa kupewa yanafikiwa na wale ambao hawajapata wapate,".

Mjema amesema kutolewa kwa vishikwambi hivyo ni mwendelezo wa jitihada za serikali kuwawezesha na kuwajengea uwezo walimu kuwa na vitendea kazi na kuimarisha matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).