Jumatatu , 21st Nov , 2022

Wizara ya Maliasili na Utalii imeeleza kuwa inathamini afya ya mama na mtoto kupitia mapato ya utalii yanayotokana na maeneo yaliyohifadhiwa ambapo kwa sasa inachangia zaidi ya asilimia 17 ya pato la Taifa.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mtoto Njiti Duniani yaliyofanyika katika kijiji cha Robanda wilaya ya Serengeti mkoani Mara.

Akizungumza wakati wa maadhimisho hayo yaliyoambatana na matukio mbalimbali ya wadau kuchangia fedha na vifaa kwa ajili ya kuhudumia watoto njiti yakiongozwa na Taasisi ya Doris Mollel (DMF), Naibu Waziri Mhe. Mary Masanja ameeleza kuwa Wizara ya Maliasili na Utalii imekua ikishiriki moja kwa moja katika kuchangia maendeleo katika maeneo mbalimbali likiwemo eneo la afya ya mtoto.

Ameipongeza Taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF) kwa kuweza kuandaa matukio mbalimbali likiwemo la kurusha balloon katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa lengo la kuitangazia dunia kuwa inamtambua na kumthamini mtoto njiti na kuonesha kwamba thamani hiyo inaweza kuonekana kupitia mchango mkubwa wa Sekta ya Utalii hapa nchini.