Jumanne , 10th Feb , 2015

Zaidi ya wanawake 2,000 wa Mkoani Dodoma wanatarajiwa kupima saratani ya matiti na ya shingo ya kizazi katika zoezi linaloendeshwa na madaktari bingwa wa saratani kutoka katika hospitali ya Ocean Road ya Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Fatma Ally.

Akizungumza katika uzinduzi wa zoezi hilo linalofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere mjini hapa, Kamanda wa UVCCM Wilaya ya Dodoma Mjini ambaye pia ndiye mfadhili wa zoezi hilo, Haidari Gulamali amesema ameamua kufadhili upimaji wa saratani hizo kwa wanawake kwa kuwa wanawake wengi wanaishi bila kujijua afya zao.

Amesema wataalamu wa saratani kutoka katika hospitali ya saratani ya Ocean Road wamekubali kuacha majukumu yao mengine na kuamua kutoa vipimo bure kwa akina mama wa Mkoa wa Dodoma ili kupunguza kasi ya ugonjwa wa saratani kwa wale watakaogundulika kuwa na dalili mapema.

Kwa upande wake kaimu mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Fatma Ally aliwataka wanawake mkoani Hapa kuhamasishana ili wote kwa pamoja waweze kupima afya zao na kuweza kupata matibabu kwa wale ambao watagundulika kuwa na matatizo.