Kituo cha uwekezaji chatoa taarifa yake

Alhamisi , 29th Apr , 2021

Kituo cha Uwekezaji nchini TIC kimesema kuanzia Julai 2020 hadi sasa hakuna kampeni iliyofanyika ya kusafiri kutangaza vivutio vya utalii kutokana na mataifa mbalimbali duniani kuweka masharti dhidi ya Covid 19 hali iliyopelekea kuendesha mikutano zaidi ya saba kwa njia ya mtandao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji nchini Dkt Maduhu Kazi

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Uwekezaji nchini Dkt Maduhu Kazi wakati akitoa Taarifa ya robo ya tatu ya mwaka 2020/2021 ambapo pia ameelezea hadi sasa jumla ya miradi 151 imesajiliwa katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi machi 2021.

"Kama Kituo kwa sasa tunafanya kila mbinu kuhakikisha zile changamoto zote za Uwekezaji zinakoma ikiwemo upande wa ardhi,ushirikiano katika Taasisi zinazoingiliana katika Uwekezaji," amesema Dkt Maduhu.

Aidha Dkt Kazi ameeleza kuwa wamekuwa wakitumia jukwaa la Africa Investment Forum kuielezea miradi ya ndani  kwakuwa pana wafanyabiashara na wawekezaji wakubwa kutoka duniani .

Kuhusu Suala la wawekezaji wanaohitaji ardhi amesema wanashirikiana vyema na wizara ya ardhi kuhakikisha wanapata maeneo bila vikwazo huku Taasisi ikiboresha utoaji wa huduma za vibali na leseni katika Kituo Cha pamoja yaani one stop facilitation center.