Alhamisi , 14th Jul , 2016

Shindano la Dance 100 linaloratibiwa na kampuni ya EATV linatarajia kuanza kwa kishindo katika viwanja vya Leaders Club Jijini Dar es salaam ambapo mwaka huu ni msimu wa tano tangu kuanzishwa mwaka 2012.

Maneja uhusiano wa Vodacom Tazania Bwn. Matina Nkurlu (wa katikati) akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari meneja wa uhusiano wa Vodacom Tanzania Matina Nkurlu amewataka vijana nchini kuchangamkia fursa ya shindano hilo ambapo vijana wengi wanaweza kupata ajira kupitia shindano hilo.

‘’Vijana jiungeni kwenye vikundi na mjitokeze kwa wingi kwani kupitia shindano hili ukiachilia mbali zawadi ambazo tumekuwa tukitoa lakini wasanii mbalimbali hushiriki kuchukua vijana mbalimbali kwa ajili ya kucheza katika kazi zao, ndiyo maana Vodacom tukaona tushiriki katika kusaidia vijana kuweza kutumia fursa hii kujiajiri hivyo hii ni fursa yenu ya kipekee’’ Amesema Nkurlu.

Kwa upande wake mmoja wa waratibu wa shindano hilo kutoka EATV Brendansia Kileo amewataka vijana kuondoa woga kwani shindano hilo limeweza kuwa na mafanikio makubwa kwani vijana wengi wamechukuliwa na bendi na washiriki wa shindano hilo wameweza kushiriki mashindano mengine na kuibuka washindi kama The chocolate (2013) Wakali sisi (2014) na WD (2015)

Mmoja wa majaji wa muda wa shindano hilo Super Nyamwela amesema shindano la mwaka huu linatarajiwa kuwa na muamko wa aina yake ukilinganisha na mwaka jana kutokana na hamasa ya shindano hilo kushika kasi ndani ya jamii.
Jaji mwingine Khalila Mbowe amewataka kinadada kujitokeza kwa wingi na kuwasihi wazazi kuwapa ruhusa vijana wao kwani shindano hilo litaweza kubadili maisha ya watoto wao , na kuwaasa vijana kujipanga vilivyo ili kuibuka kidedea.

Aidha mashindano ya mwaka huu yataanza raundi tatu za usaili utakaofanyika tarehe 13, 23 na 30 Julai na kufuatiwa na robo fainali, nusu fainali na fainali . Vipindi vya shindano hili vitarushwa kila siku ya jumapili saa moja usiku, na mashindano haya yayana kiingilio cha usaili.

Tags: