Jumatano , 3rd Aug , 2016

Kundi la Best Boys ambalo limeshiriki shindano la Dance100% mara ya tano mfululizo limesema kwa mazoezi ambayo wanayafanya kila siku na ubunifu ambao wanauonesha kwenye shindano hilo hawawezi kushindwa kwa kuwa wameshatambua ubunifu ndiyo nyenzo kuu

Kundi la 'Best Boys Kaka Zao'

Akizungumza na EATV kuhusu namna walivyojipanga katika shindano la Dance100% mwaka huu baada ya kuibuka kidedea katika nafasi tano zilizotafutwa katika usaili wa mwisho TCC Chang’ombe, Mwenyekiti wa kundi hilo Edy Brilliant amesema kundi lao limejisahihisha vya kutosha na mwaka huu ubunifu wa kazi yao ndiyo utakuwa kivutio kikubwa cha kuwezesha kushinda.

‘’Sisi hatuna mbwembwe sana jukwaani bali tuna ubunifu ambao tunautumia ili kuonesha utofauti na makundi mengine kwa maana makundi mengi yamekuwa yakirudia vitu, jambo ambalo linakosesha alama wakati majaji wanapokuwa wanatizama show’’ Amesema Edy.

Shindano la Dance100% baada ya kumaliza hatua ya kwanza muhimu ya usaili wa awamu tatu, kilichobakia ni shindano kuelekea katika nafasi ya robo fainali ambayo itafanyika Agost 13, 2016 katika viwanja vya Don Bosco Osterbay Jijini Dar es Salaam.

Aidha matukio yote ya Dance100% yanaoneshwa kila siku ya Jumapili saa moja jioni kupitia EATV chini ya udhamini maridhawa wa Vodacom na Coca-Cola.

Tags: