Jumatano , 21st Feb , 2018

Msanii wa filamu nchini Irene Uwoya amefunguka na kudai kuna baadhi ya wanawake wamekuwa na tabia ya kuwakatisha tamaa wenzao katika vitu ambavyo wanavifanya na kupelekea wanaume ndio wanawapa ushirikiano kwenye masuala yao jambo ambalo sio zuri.

Uwoya ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii baada ya kuwepo tabia hiyo kwa muda mrefu katika jamii, ofisini na sehemu nyingine. 

"Hivi kwanini wanawake tunakuwa hatupendani, yani najiulizaga sanaaa badala sisi tushirikiane ndio kwanza tunarudishana nyuma. Mtu akifanya kitu kizuri au biashara ndio wa kwanza kuponda na kurudishana nyuma", amesema Uwoya.

Pamoja na hayo, Uwoya ameendelea kwa kusema "yani unamskia mtu kabisa anakuponda mbaya halafu hujawahi hata kugombana nae na pengine unamsaidiaga tu sana. Yani unashanga wanaokuunga mkono ni wanaume badala ya wanawake wenzako, halafu ukifanya mabaya ndio anakusifia balaaah ili uwendele kuharibu".

Aidha, Uwoya amesema kwamba pindi ikitokea kwa watu wa aina hiyo wameanzisha biashara yake basi yeye ndio huwa anapenda kuungwa mkono huku akijisahau kwamba yeye hakuwahi kuwasaidia wenzake katika masuala hayo

"Nimeamua sasa hivi nisi-support mtu yeyote asie ni-support na haina haja ya kuleana kabisa mtu asie kuwa na umuhimu kwenye maisha yako haina haja ya kuwa sehemu ya maisha yako atakurudisha nyuma tu. Achana na watu wasio na faida wala mchango wowote kwenye maisha yako", amesisitiza Uwoya.

Kwa upande mwingine, Uwoya amewashauri wanawake wenzake na jamii kwa ujumla kutokuwa na marafiki ambae muda wote anakushauri kufanya starehe badala ya kukupa fikra za kutengeneza biashara ili uweze kupata fedha.