Ijumaa , 15th Dec , 2017

Baada ya msanii wa Hip Hop Kala Jelemiah kula shavu la nguvu la kusifiwa na Makamu wa Rais Mama Samia Suluhu kuwa ngoma yake mpya aliyoachia hivi karibuni “Kijana” ni nzuri, amesema anajipanga kuilipa heshima hiyo aliyopewa na kiongozi wa nchi.

Akiongea kupitia eNEWZ ya     East Africa Television Kala amesema "nimefanya mziki kwa mda mrefu ila sijawahi kupata pongezi kutoka kwa kiongozi mkubwa wa nchi kama yule tena mbele za maelfu ya watu mara nyingi tumekuwa tukikutana na viongozi wa kawaida na kutupa pongezi za kawaida”.

Kala ameongeza kuwa alizipokea salamu za Makamu wa Rais kutoka kwa watu wengi  kitendo ambacho amekipokea  kwa mikono miwili na kuwa kauli hiyo ya Makamu wa Rais imempa deni la kuendelea kukaza buti na kuandaa nyimbo  nyingi  zitakazo kuwa mkombozi kwa Jamii.

Kala amemaliza kwa kusema  kauli ya Makamu wa Rais imempa faraja yeye na familia yake kwa ujumla na hata alipotumiwa kile kipande cha video ambayo Makam wa Rais alikuwa anamsifia aliiangalia mara nyingi kiasi kwamba hakuamini kitu ambacho alikuwa anakiona.

Msanii huyo wa Hip Hop kutoka Rock City anafunga mwaka kwa kauli yake ya kuwa hakuna mziki wa biashara bali kuna biashara ya muziki aliyoitoa hivi karibuni kupitia Enewz.