Jumatatu , 21st Sep , 2015

Baada ya mpambano wa kukata na shoka, hatimaye makundi matano ya kudansi Team ya shamba, Best Bo

Baada ya mpambano wa kukata na shoka, hatimaye makundi matano ya kudansi Team ya shamba, Best Boys, Team Makorokocho, The WD na The winners wamefanikiwa kuingia fainali ya mashindano makubwa ya Dance 100% (2015), baada ya kufanikiwa kujivunia alama zaidi katika mashindano hayo yaliyofanyika Don Bosco Oysterbay jijini Dar es Salaam siku ya juzi (Jumamosi).

Ushindani mkali ulionyeshwa na washiriki wote juu ya jukwaa la kisasa, ubunifu katika mitindo ya kucheza na mavazi kwa makundi hayo ukiwa ni kiburudisho kingine kikubwa kwa umati mkubwa uliohudhuria mashindano hayo.

Hisia nzito na huzuni vilitawala wakati wa kutangazwa kwa washindi, na kufikia wengine kupoteza fahamu hususana kwa makundi, ambayo hayakuweza kupenya wakiwepo Cute Babies, Quality Boys, The Best, Wazawa Crew na Majokeri.

Katika kuzingatia vigezo, haki, umakini na kusimamia sheria katika ubora wake hadi kuhakikisha washindi waliopatikana wanastahili, dawati la waamuzi ambalo limezoeleka kuendeshwa na majaji Super Nyamwela, Queen Darleen pamoja na Shetta liliongezeka majaji wawili wapya, Mwalimu mahiri wa Dansi Kalila Mbowe na Lydia Igarabuza kutoka EATV.

Baada ya mzunguko huo, sasa macho ni kwenye hatua ya fainali ambapo mabingwa wapya wa kombe la Dance 100% watapatikana na kuheshimika kama wafalme wa dansi Tanznia. Vilevile mabingwa hao watashinda zawadi tofauti ikiwemo kitita cha fedha taslim shilingi milioni 5 za Tanzania. Swali kubwa likibaki kuwa ni kundi gani litakaloibuka na taji hili na kitita hicho mwaka huu.

Usikose kutazama kila kilichojiri katika hatua ya Nusu Fainali ya mashindano hayo yaliyoshereheshwa kwa uzuri kabisa na T Bway 360 na Maggie Vampire kwa kutazama kipindi cha Dance 100% kupitia EATV pekee, Jumamosi saa 12:30 jioni.

Safari inazidi kukaribia ukingoni kuelekea hatua ya fainali ambapo mashindano haya makubwa yanaletwa kwako na East Africa Television na East Africa Radio kwa udhamini mkubwa wa Vodacom Tanzania, na pia Cocacola kinywaji rasmi cha Dance 100% kwa mwaka huu kinachokupa sababu Bilioni za kujiamini.

Ni Burudani mwanzo mwisho, Dance 100% (2015).