Ijumaa , 16th Nov , 2018

Msanii wa filamu nchini aliyekuwa akikabiliwa na kesi ya kuua bila kukusudia, Elizabeth Michael (Lulu) amefunguka kwa mara ya kwanza baada ya kuachiwa huru Novemba 12.

Msanii Elizabeth Michael (Lulu).

Kupitia ukurasa wake wa 'Instagram' Lulu ametoa shukurani kwa kila aliyeshiriki kumuombea na kumshika mkono kwa namna yoyote ile katika kipindi chake chote cha kesi yake.

Lulu ameandika, "Kwa dhati kabisa nichukue nafasi hii kumshukuru kila aliyeshiriki kuniombea katika kipindi kigumu sana kwangu, kwa familia yangu na watu wangu wa karibu, mliolia na kusali pamoja na mimi ni wengi mno, ninaowajua na nisiowajua".

Ameongeza kuwa, "Kilikuwa kipindi chenye maumivu, matusi, dharau, hukumu za wanadamu, maneno ya kulaaniwa, majina yasiyofaa na mambo mengi ya aina hiyo, lakini nashukuru Mungu sikuyapokea kama yalivyo bali niliyapokea kama shule au somo lililojaa utukufu wake".

Lulu ameendelea kwa kusema kuwa kile kilikuwa ni kikombe na ilikuwa ni lazima akinywe, yalikuwa majira ambayo ni lazima ilikuwa apitie na mwisho yakawa mapenzi ya Mungu na yametimizwa.

Lulu alikuwa akitumikia kifungo cha miaka miwili jela, baada ya Novemba 13, mwaka jana kuhukumiwa na mahakama kuu baada ya kupatikana na hatia ya kumuua bila kukusudia aliyekuwa gwiji wa filamu, Steven Kanumba.

Hata hivyo, Aprili 26 mwaka huu, msanii huyo alibadilishiwa adhabu hiyo na kuwa ya kifungo cha nje. Kutokana na hilo, alipangiwa kazi ya kufanya usafi katika Wizara ya Mambo ya Ndani iliyopo maeneo ya Posta Jijini Dar es salaam aliyoianza tangu Mei 14 mwaka huu.