Jumapili , 17th Jul , 2016

Mashindano ya kusaka vipaji kwa vijana wenye uwezo wa kucheza maarufu kama Dance100% msimu wa mwaka huu 2016 yameanza jana katika viwanja vya Leaders Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali.

Kundi la Mafia Crew lilipokuwa likionyesha uwezo wao shindano la Dance100%

Shindano hilo ambalo limeanza mwaka 2012 mwaka huu linaendelea kwa msimu wa tano ambapo vijana hujiunga katika makundi ya watu watano hadi nane na kufanya mazoezi na kIsha kuonesha vipaji vyao siku ya usaili, ambapo majaji maalum wenye weledi wa kazi hiyo hufuatilia kazi hiyo na kutoa alama kwa washiriki.

Kwa siku ya jana makundi 10 yamejiandikishwa ambapo makundi yaliyoweza kuibuka kidedea ni makundi matano ambayo yataendelea kujifua huku yakisubiri usaili awamu mbili zijazo ndiyo yatinge kwenye robo fainali.

Shindano la mwaka huu linadhaminiwa na kampuni ya Vodacom kwa kushirikiana na kinywaji baridi cha Coca-Cola ambapo mshindi wa kwanza mwaka huu ataibuka na kitita cha milioni 7 ambapo zawadi hiyo imeongezeka ukilinganisha na mwaka jana ambapo zawadi ilikuwa ni milioni tano kwa mshindi wa kwanza.

Aidha mashindano haya hayana kiingilio katika usaili wake hivyo vijana wanaruhusiwa kujitokeza kadiri ya uwezo wao na shindano litakuwa likirushwa na kituo cha EATV kila siku ya Jumapili saa moja usiku.

Makundi matano yaliyoingia tano bora hapa Leaders Club ni Mafia Crew, The DDI Crew, BBK Boys, Mazabe Powder, Tatanisha Crew

Tags: