Mr. Nice amkana Young D

Thursday , 7th Dec , 2017

Msanii mkongwe wa muziki wa bongo fleva kwenye miondoko ya TAKEU, Mr. Nice, amesema hamjui msanii Young D ambaye ametumia wimbo wake, na kwamba hakubaliani na kitendo cha yeye kutumia kazi yake.

Akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, Mr. Nice amesema licha ya kutoruhusu mtu yeyote kutumia kazi zake, hajapata taarifa kutoka kwa Young D wala uongozi wake, na hajawahi kumjua kwenye maisha yake.

"Sijawahi kuongea wala kuruhusu binadamu yoyote kutumia kazi yangu yoyote bila makubaliano na ridhaa yangu mwenyewe iwe ni kwa kuniheshimu ama kunidhihaki, so far simjui huyo Young D at all , ndo namsikia kwako", amesema Mr. Nice.

Kwa upande wa Young D amesema suala hilo tayari uongozi wake unalishughulikia ili kumalizana na malalamiko ya Mr. Nice, hata hivyo aliamua kufanya kama kumpa heshima kutokana na kukubali kazi zake alizokuwa akizifanya.