Jumanne , 12th Dec , 2017

Msanii Mwana FA ambaye hivi karibuni amemaliza tofauti zake na msanii mwenzake lady Jaydee, ameweka wazi jibu la kitendawili ambacho wengi walikuwa wakijiuliza, juu ya chanzo cha ugomvi wao uliowapelekea kuwa mahasimu.

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Mwana FA amesema chanzo kikubwa cha ugomvi wao ilikuwa ni kupangwa kwa show zao kwa siku moja, kitu ambacho kilionekana kumkwaza mmoja wapo.

Sababu kubwa ilikuwa ni show yake na yangu zilianguka tarehe moja , nilikuwa na mipango ya show yangu na nilimwambia, hakuwa na neno, sasa mipango inavyoenda haiendi kwa kalenda yako inaenda kwa kalenda ya wadhamini, bahati mbaya Mangwea akafariki, wote tukaghairisha tukapeleka tarehe 31 na yeye na team yake wakasogeza mpaka 31, na wala haikupangwa kwa sababu yeye alipanga tarehe hiyo hiyo, mimi sikuona kitu kibaya kwa sababu Dar es salaam ina watu zaidi ya milioni 6, mimi nilikuwa nahitaji watu 400 tu nikaona haina tatizo, unajua tumeumbwa binadamu tuko tofauti tutachukulia ubaya, baada ya hapo maneno yakawa yameanza, ila hakukuwa na sababu nyingine zaidi ya hiyo”, amesema Mwana FA.

Kwa muda mrefu wasanii hao walikuwa hawapikiki chungu kimoja, huku wengi wakiwa wanajiuliza nini chanzo cha wawili hao kutoelewana ilhali walikuwa marafiki wakubwa wa kupika na kupakua, na kuja kumaliza tofauti zao mwaka huu.