Jumamosi , 13th Aug , 2016

Jaji mkongwe wa shindano la Dance100% Super Nyamwela amesema amefurahishwa na namna vijana wanavyozidi kuimarika katika sanaa ya uchezaji nchini hasa kupitia shindano la Dance100% 2016.

Jaji mkongwe wa shindano la Dance100% Super Nyamwela

Nyamwela ameyasema hayo mara baada ya kumaliza kibarua cha kutizama na kutoa alama katika hatua ya robo fainali ya shindano la Dance100% hatua ya robo fainali iliyofanyika katika viwanja vya Don Bosco Jijini Dar es salaam.

“Kwa kweli vijana wakielekezwa wanaweza kufanya vizuri sana kwa siku kadhaa majaji tumefanikiwa kuwatembelea washiriki katika maeneo yao wanayofanya mazoezi na kuwaelekeza mbinu za kuweza kufanya vizuri zaidi na mambo ambayo yanahitajika katika sanaa ya uchezaji hasa kuzingatia muda, kuonesha vitendo, kutawala jukwaa pamoja na kuwa nadhifu mbele ya watazamaji” Amesema Nyamwela.

Nyamwela ameongeza kuwa jamii inapaswa kutambua kwamba sanaa ya kucheza inalipa kama vijana wakiwa na ubunifu na kujituma kwani kupitia sanaa hiyo itawafanya watambulike na kupata kazi mbalimbali kwenye sherehe, kushiriki mashindano mengine ndani ya jamii pamoja na kuchukuliwa na bendi mbalimbali kuweza kufanya nao kazi jambo ambalo litapunguza idadi ya vijana tegemezi ndani ya jamii.

Aidha katika shindano la robo fainali makundi 10 yameweza kushinda na kutinga hatua ya nusu fainali ambapo kupitia EATV watazamaji wanaweza kufuatilia hali nzima ya shindano ilivyokuwa kila siku ya Jumapili saa moja kamili jioni.

Tags: