Stamina afunguka kusalitiwa na mkewe

Alhamisi , 9th Jan , 2020

Baada ya kuachia wimbo wake wa asiwaze ambao amezungumzia misukosuko ya ndoa yake, EATV & EA Radio Digital, imempata msanii Stamina na amesema vyote alivyoimba vimetokea kwenye uhalisia wake na lazima maisha yaendelee.

Stamina akiwa na mke wake siku ya harusi yao

"Mimi ni msanii kama kuna kitu kimenitokea najua hata kwenye jamii yangu kipo, nilichokiimba kina uhalisia kwangu na kwenye jamii, sioni mipaka mimi kama fanani kuwasilisha fasihi yangu kwa watu, hivi vitu vipo mtaani hata kama hakijanitokea mimi kuna watu vinawatokea" ameeleza Stamina.

Aidha Stamina ameendelea kusema "Ukisikiliza nyimbo ambayo ipo katika historia ya kweli ya maisha, utaelewa nini ambacho kinaendelea sina haja tena ya kueleza, kama kimetokea nini au tumefanya nini na siwezi kwenda kwenye vyombo vya habari na kumuongelea mtu vibaya".

Pia akizungumzia kuhusu mke wake kumsaliti na kutembea na aliyekuwa mchezaji wa klabu ya Simba kama alivyoimba kwenye wimbo wake, Stamina amesema "Hii ni kazi ya fasihi siwezi kusema kwamba mchezaji fulani ametoka na mke wangu, ila ninaweza nikawasilisha kitu kingine tofauti kama usaliti na sio lazima iwe hivyo kama watu wanavyofikiria"