Jumamosi , 13th Aug , 2016

Kundi linaloshiriki kwa mara ya pili katika shindano la Dance100% 2016 Makorokocho Crew limesema lisiposhinda shindano la mwaka huu kwa namna walivyojipanga na kufuata maelekezo ya majaji na mazoezi ya kila siku, hawatashiriki tena shindano hilo.

Kundi la Makorokocho Crew lilipokuwa likionesha ufundi katika shindano la Dance100% Robo Fainali

Akizungumza na EATV Mwenyekiti wa kundi akiwa pamoja na wenzake amesema wameafikiana kwamba kwa ufundi wanaouonesha mwaka huu wakishindwa tena basi itakuwa hawana bahati ya kushinda shindano hilo na wataamua kuendelea na sanaa ya uchezaji lakini siyo kwa shindano hilo.

“Kwa juhudi tulizo nazo na namna tunavyowasikiliza majaji na kufanyia kazi maelekezo yao milioni 7 ya mwaka huu ni ya kwetu na kama tusipo ipata tumekubaliana tuache kushiriki kwa sababu tunatumia nguvu nyingi na gharama kubwa kuhakikisha tunashinda mwaka huu na tumejipanga siku nyingi na kila siku tunafanya mazoezi”Amesema Salum Abas Mwenyekiti wa kundi.

Kwa upande wake Hamadi au kwa jina lingine la usanii Chenga amesema mwaka wa pili waliishia fainali hivyo makosa ya mwaka jana wameweza kuyafanyia kazi na kuhakikisha kwamba mwaka huu wanaonesha kipaji cha hali ya juu na ushindi upo kwao.

“Tunafahamu haya ni mashindano na sisi tumekuja kushindana ila tunaamini tumewazidi wenzetu sana ndiyo maana tumesema kama tusiposhinda mwaka huu sisi tutawaachia wengine washiriki tuendelee na mishe mishe zetu nyingine” Amesema Hamadi.

Kuhusu uamuzi wa Team Makorokocho kusema hawatashiriki tena wasiposhinda mwaka huu, Jaji Super Nyamwela amesema majaji wote wa shindano hilo wanasimamia vigezo na masharti hivyo kundi litakalofanya vizuri ndilo litaibuka na ushindi hivyo kundi hilo lifanye vizuri kwa kuzingatia vigezo, majaji watatenda haki kwa wote.

Tags: