Alhamisi , 24th Mar , 2016

Kama ambavyo nilianza kuwaletea uchambuzi wa tungo mbali mbali za muziki wa reggae, leo naendela na zile tungo ambazo nadhani wasanii wetu wakifahamu kuhusu hili, watajifunzi kitu cha msingi sana.

“Waambie ukweli vijana wajue asili yao, wajue historia yao na kwamba tulilazimishwa kuja”. Hayo ni maneno ya Hayati Jimmy Riley kwenye wimbo wa Tell youth the truth, ambao leo ni moja ya tungo ambazo nitazielezea, zilizoimba kuhusu uafrika na jinsi gani wasanii wakongwe wa reggae wanajivunia kuwa na asili ya bara hili la Afrika.

Kama inavyofahamika wasanii wengi wa muziki wa reggae asili yao ni Jamaica, lakini wenyewe wanalipinga hilo kwa nguvu zote wakisema Jamaica ni uhamishoni tu, na Afrika ndio nyumbani kwao.

Kama nilivyoanza kwa msanii Jimmy Riley ambaye ni baba mzazi wa msanii wa reggae Tarrus Riley, aliyekutwa na umauti hivi karibuni, kwenye wimbo wa Tell youth the truth, amesema huku tuliko tulilazimishwa kuja, wafungwa tuliolazimishwa kwenda.

Kauli hiyo ya Jimmy Riley inakuja kupigiwa mstari na Jepther McClymont maarufu wa jina la Luciano, ambaye ni maarufu sana mpaka sasa kutokana na tungo zake zenye ujumbe mzuri, huku wengi wakisema msanii huyo haimbi muziki wa reggae, bali huimba muziki wa injili kwenye mahadhi ya reggae, kwa kibao chake cha 'When will I be home', anasikika akisema “kila muda naangalia nafsi yangu na kujisemea mwenyewe, nitaenda kuogelea kwenye mto Nile, muda mwingi siwezi kutafsiri ila ndio najua mimi ni mtoto wa Afrika, walitubeba ughaibuni, bado natamani kurudi nyumbni, na muda mwengine nawaza lini nitakuwa nyumbani”. Hayo ni baadhi ya maneno yaliyosikika kwenye wimbo wa Luciano When.

Luciano anaendelea kusema wakati mwingine nawaza lini nitakuwa tena nyumbani, niweze kuoga kwenye mto Nile mimi na wewe rafiki yangu, huku akitaja nchi mbali mbali za Afrika ikiwemo Tanzania, Nigeria, na nyinginezo.

Kutajwa kwa nchi kama Tanzania kwenye muziki wa mtu kama Luciano ni ishara kubwa kuwa wanatambua vilivyo bara la Afrika na nchi zake, pia hata na rasilimali zake ikiwemo mto Nile, ambao ndio mto mrefu duniani.

Lakini maswali ya Luciano yanatulizwa na nguli mkongwe wa muziki wa reggae ambaye pia ni muasisi wa bendi ya The Wailers, mwenye utaalamu wa kucheza vyombo vyote vya muziki Peter Tosh, kwenye wimbo wake wa African, anasema haijalishi umetoka wapi, ili mradi wewe ni mtu mweusi basi wewe ni Mwafrika, usijali utaifa wako, una utambulisho wa mwafrika, kauli ambayo inaungwa mkono na watu wengi duniani wenye ngozi nyeusi, ambao asili yao ni Afrika.

Lakini wakati wengine wakijiuliza na wengine kujigamba kwamba wao waliko ni ugenini na nyumbani ni Afrika, Msanii ambaye kwa upande wangu namuona ni msanii mzuri zaidi wa muziki wa reggae kwa sasa kati ya waliobaki, Nasio Fontaine, amekata shauri na kusema narudi nyumbani, huku akitaja jinsi walivyouzwa na kutawanyika duniani na kusema ooh Afrika narudi nyumbani. Wimbo huu mtamu wa Nasio Fontaine unaoitwa 'Wanna go home' kuna mahali anathibitisha kuwa hapa nakuona, Afrika kwa Waafrika, nyumbani na ughaibuni akimaanisha kwa kule aliko sasa (Jamaica) anaiona Afrika kama ughaibuni laikini ndio nyumbani . (Wanna go home,So here I seh, yeah! “Africa for Africans, A home and abroad”, So man must go home, ye-ah! )

Bila kumsahau Winston Rodney OD au BurningSpear, kitu ambacho kwanza kinanifurahisha ni kutokana na tungo zake zenye ukweli wenye kukufunua ufahamu wako na zenye kufurahisha, lakini pia hajaacha kusema chochote kuhusu mama Afrika. Kwenye wimbo wake wa Afrika Burning Spear anasema tunaenda huko, kwenye utambulisho wetu wa kweli, huku akisikika akiutaja mlima Kilimanjaro ambao upo hapa nyumbani Tanzania.
(Call his MajestyWe go de, we go de, Call Him!Tell him we found our names of age
We go de, we go de, we go de,Our true identity, We go de, Kilimanjaro,We go de, we go de, we go de )

Kitu kingine cha Kujivunia pia kwa sisi watanzania ni kwa wasanii hawa kuutangaza mlima Kilimanjaro, na dunia nzima kujua kuwa Afrika kuna mlima Kilimanjaro ulipo Tanzania, jambo ambalo sidhani kama wasanii wetu wa sasa wanaweza kusimama kifua mbele na kusema hilo.

Nikirejea kwa mwenyewe God father wa muziki wa reggaeRobert Nesta Marley 'Bob Marley' ingawa wapo waliomzidi, kama haufahamu endelea kubaki nasi utajua ni msanii yupi alimzidi Bob Marley na alimzidi nini, isipokuwa kile alichokiita msanii wa muziki wa kizazi kipya wa bongo Fleva Diamond Platnums, 'nyota' yake ndio ilimzidi na kumfanya Bob Marley akubalike dunia nzima kuwa ndiye baba wa muziki wareggae, hakuacha kuimba kuhusu Afrika, tena zipo tungo nyingi zinazohusu Afrika, lakini hapa nitazungumzia wimbo wa 'Afrika Unite', anasema Africa Unite coz the children wanna come home. Wimbo huu alisisitiza kipindi kile umoja wa nchi za Afrika unaundwa na kudai uhuru wa nchi hizo, akiwaasa waafrika waungane kwa upendo ili hata wale walioko ughaibuni warudi nyumbani, ni wimbo mtamu sana ukiusikiliza na ukaelewa ujumbe wake.

Kwenye wimbo huu kuna mahali anasema ('Cause we're moving right out of Babylon,
And we're going to our Father's land, yea-ea.) akimaanisha tunaondoka kwenye mfumo wa kibabylon (Babylon kwa lugha ya kirasta ni mfumo dhalimu wenye kunyanyasa watu wake) na tunaenda kwenye ardi ya baba yetu, alisikika Bob Marley kwenye Afrika Unite.

Kuna mengi ya kujifunza kutoka kwenye hizi tungo chache nilizozielezea leo, uzalendo wa kujitambua wewe ni nani, kujikubali asili yako. Siku hizi vijana wengi tunaukataa uafrika wetu na kuiga umgharibi tena ule usio na tija, na matokeo yake tunaanguka kwenye matatizo ya maadili na jamii kuharibika kisaikolojia. Kumbukeni Lucky Dube aliwaonya kwenye 'The Other side', aliposema majani ni ya kijani sana kwa upande wa pili, lakini mpaka utakapofika huko ndipo utajionea mwenyewe.

Lakini tujiulize kitu hapa, ni kweli Afrika wanayojivunia ndiyo iliyopo!? kuna mambo mengi upande wa pili wa bara hili la Afrika, uhalisia wa maisha ya watu wake, na yale yaliyopo kwa ajili yao.

Endelea kuwa nasi.