Jumanne , 18th Dec , 2018

Msanii wa filamu bongo Wastara Juma ameiomba serikali kumsaidia kupata gari lake, ambalo limezuiliwa bandarini kutokana na kutolipiwa ushuru.

Akizungumza na www.eatv.tv, Wastara amesema kwamba gari hilo alipewa msaada na mtu kutoka Japan, lakini anashindwa kulipata kutokana na kutokuwa na uwezo wa kulipia ushuru.

Ameendelea kusema kuwa ameshahangaika mpaka kwa vyama vya walemavu kuweza kupata msaada, lakini imeshindikana huku wakimtaka alipie gari hiyo au iwe gari maalum ya walemavu.

“Sina uwezo wa kutembea mwendo mrefu, kuna mtu ametoka huko Japan akasema mimi nakusaidia gari, akaona kwa biashara ninazofanya litanisaidia, kweli gari ikatumwa, nikahangaikia usafiri gari ikafika, mimi kama mlemavu nikahangaika kwenye vyama vya walemavu vinisaidie lile gari nilipate free, ushuru wake ni milioni 6 hadi 7, vyama vya walemavu wameshindwa kunisaidia, wakaniambia mpaka iwe gari ya walemavu, sasa mtu kataka kunisaidia tu mpaka nimpangie liwe la walemavu, kama gari zilijaa kwenye yard yake”, amesema Wastara.

Wastara aliendelea kuwa, “Sina uwezo wa kuligomboa nabaki kuliangalia tu, mpaka kwa waziri nimefika anisaidie, sasa mimi sioni msaada, nakaa nawaza, mambo kama haya unaweza kuta mtu kafa ghafla kwa sababu nina mlundikano wa mawazo, niwaombe wanisaidie kulitoa gari langu, niwaambie hili gari ni la msaada".

Licha ya hayo yote Wastara amesema iwapo atalipata gari hilo litamsaidia, kwasababu ana familia kubwa anayoilea, wakiwemo watoto wake na watoto wengine ambao si wake.