Watoto watatu wapotea mazingira ya kutatanisha

Jumamosi , 2nd Nov , 2019

Watoto watatu wakiwamo wawili wa familia moja wamepotea katika mazingira ya kutatanisha katika kijiji cha Kalonge, kata ya Ibwera, halmashauri ya Bukoba vijijini, mkoani Kagera.

Tukio la watoto watatu kupotea mkoani Kagera

Leo ni siku ya tano tangu watoto hao watoweke nyumbani kwao Oktoba 28 mwaka huu, na taarifa kutoka kijijini hapo zimedai kuwa walimfuata dada yao aliyeondoka kwenda kuchanja kuni porini, ambaye hata hivyo aliporejea alidai hajawaona.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi mkoani Kagera, Revocatus Malimi amewataja watoto hao kuwa ni Anisia Geofrey mwenye umri wa miaka sita, Byarugaba Prasidius mwenye umri wa miaka mitano, ambao ni wa familia moja waliokuwa wakilelewa na babu yao, huku akimtaja mtoto wa tatu kuwa ni Jamal Kamugisha mwenye umri wa miaka mitatu ambaye ni mtoto wa jirani yao.

Baadhi ya wananchi waliozungumzia tukio hilo wamewataka wazazi kuwa makini na watoto wao kwa kufuatilia mazingira wanayochezea ili kuhakikisha kama wako salama.