Jumapili , 22nd Sep , 2019

Mbunge wa Jimbo la Segerea, Bonnah Kamoli amesema sio Wabunge wa Upinzani pekee, ambao huwa wanafukuzwa Bungeni hata Wabunge wa Chama Cha Mapinduzi huwa wanapelekwa Kamati ya Maadili, lakini wao huwa hawasemi.

Bonnah Kamoli ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye kipindi cha Kikaangoni, kinachorushwa kupitia kurasa za Facebook na Youtube za EATV, wakati akijibu swali juu ya kitu gani ambacho kinamkera sana ndani ya Bunge la sasa, linaloongozwa na Spika Ndugai.

Bonnah Kamoli amesema kuwa "sio Wabunge wa Upinzani peke yake ambao wanafukuzwa hata Wabunge wa CCM na wao wanafukuzwa ambao walileta utovu wa nidhamu, na hata Masele aliombewa msamaha kwa sababu alikuwa tayari kuja mbele za watu kuomba radhi"

"Wapo Wabunge wa CCM wanaofukuzwa na wanapelekwa Kamati ya Maadili, lakini sisi si rahisi kuandika kwenye mitandao kuwa tumepelekwa kwenye Kamati ya Maadili, sema wenzetu ni rahisi jamii kujua, kwa sababu huwa wanaandika wasidhani na sisi hatuna matatizo ila tunaheshimu kanuni za chama chetu." amesema Bonnah Kamoli

Katika kipindi hicho Mbunge wa Segerea Bonnah Kamoli amesema anaimani anaweza akawa Rais anayefuata baada ya Rais wa sasa  Magufuli.

Tazama mahojiano kamili hapo chini.