Baba wa watoto 100 na wake 19 aongeza wake wengine

Jumanne , 15th Oct , 2019

Kutokea  katika kijiji cha Ruyonza nchini Uganda kuna taarifa ambayo imezua gumzo mitandaoni kuhusu mzee mwenye umri wa miaka 94 aitwaye Nulu Ssemakula aliyeamua kuongeza wake wengine wanne huku akiwa tayari na wake 19 na jumla ya watoto 100.

Mzee Nulu Ssemakula akiwa na sehemu ya familia yake

Mzee huyo anatokea katika kijiji ambacho sifa yake kubwa kwa wanaume ni kumiliki mwanamke zaidi ya mmoja, ambapo mawnyewe amesema lengo lake ni kuwa na familia kubwa zaidi, akiamini ni utajiri tosha na amepanga kuongeza wengine endapo ataendelea kuwa hai.

"Nilipoteza wake zangu wanne ambao waliniacha na kuniachia watoto tu, nitaendelea kuoa nikiwa hai. Nataka kuwa na watoto wengine na pia nitaoa tena kwa majaliwa ya Mwenyezi Mungu", amesema mzee Ssemakula.

"Naamini mali yangu ipo kwenye watoto na wanawake wangu, huu ndiyo utajiri wangu wa kweli",  ameongeza mzee huyo huku akionekana kujiamini.

Kwa sasa amesema anaishi na watoto wake 66, wengine wameshakuwa watu wazima wameanzisha familia zao, mtoto wake wa mwisho ana umri wa miezi 10, huku mke wake mdogo zaidi akiwa na miaka 24.