Fahamu kwanini hutakiwi kutafuta mpenzi mtandaoni

Jumanne , 9th Oct , 2018

Katika miaka ya hivi karibuni, mahusiano ya watu yamerahisishwa kutokana na mitandao ya kijamii, watu huwasiliana kutoka sehemu mbalimbali. Mtu aliyeko Tanzania anaweza kuwasiliana moja kwa moja na aliyeko Marekani, Uingereza na kokote duniani.

Picha ya mfano wa watu wakiperuzi mitandaoni

Teknolojia imerahisisha hata kwenye mahusiano ambapo watu wengi huanzisha mahusiano kupitia mitandao ya kijamii, mwanaume akimpenda msichana humfuata moja kwa moja na kumweleza na wakishakubaliana huanzisha mahusiano pasipo kuonana mbashara. 

Mapenzi ya mtandaoni yamekuwa na changamoto nyingi kiasi cha wengi kujuta kuingia. Kwa mujibu wa machapisho mbalimbali yaliyoandikwa na watalaam wa mahusiano mitandaoni, hizi hapa ni sababu za kwanini hutakiwi kutafuta mpenzi mtandaoni.

Hakuna ukweli

Katika mapenzi ya mitandaoni, usitegemee kuwa utakutana na mtu ambaye atakuambia ukweli wa maisha yake yote, hata kama ukiingia katika mahusiano naye bado kunavitu atakuwa anakuficha ni kwasababu tu mmekutana mtandanoni.

Maigizo ni mengi kuliko uhalisia

Asilimia ya watu wengi wanaopatikana mtandaoni hawaweki maisha yao halisia, wanaigiza maisha ili wasionekane ni wa nyuma. Kutokana na hilo unaweza ukampenda mtu kwa muonekano wake wa nje bila kuangalia anaishi vipi, suala ambalo linaweza kuja kukuumiza baadaye ukija kujua na kupelekea mapenzi kupungua.

Majeraha ni mengi

Hili nalo linakuja kwasababu wengi miongoni mwa wanaotafuta wapenzi mtandaoni huwa wameshaumizwa katika mahusiano yao ya nyuma, kwahiyo endapo ukianzisha mahusiano na mtu kama huyo ni wazi hamuwezi kufikia malengo yenu.

Hakuna ukaribu

Ukiwa unafikiria kutafuta mpenzi katika mitandao ya kijamii, basi jiandae kuwa na mahusiano ya umbali, kwa maana unaweza kupata mpenzi anayeishi mbali na wewe. Ni kama bahati nasibu, ambapo hujui unayewasiliana naye anaishi umbali gani na ulipo wewe.

Si mapenzi ni biashara

Hili nalo ni jambo linaloyakumba mahusiano ya mtandaoni, wapo wanawake wengi wanaoingia mtandaoni kwaajili ya kutafuta watu wenye pesa, hivyohivyo hata kwa wanaume nao wapo wanaotafuta wanawake wenye pesa na sio kwaajili ya mapenzi ya kweli. Kwahiyo ukiwa unatafuta mpenzi mtandaoni, jiandae kukumbana na vitu kama hivyo.