Jumatatu , 1st Oct , 2018

Nchini Indonesia kuna idadi nyingi ya makabila ambayo miongoni mwao mengine yakiwa makubwa yaani yenye idadi kubwa ya watu, na mengine yakiwa makabila madogo madogo kutoka sehemu mbali mbali za nchi hiyo.

Moja ya mti wenye makaburi.

Kabila la Toraja ni moja ya kabila kubwa nchini humo, ambalo limekuwa na tamaduni mbali mbali zenye kushangaza, hii ni kutokana na matendo yao kuwa ya kipekee na utofauti mkubwa na dunia inavyokwenda.

Kabila hili ambalo linapatikana kwenye makazi ya Tana, Kusini mwa Saluwesi nchini Indonesia, lenye idadi ya watu zaidi ya milioni moja..

Kabila hilo ni maarufu kutokana na mila zao ikiwemo kufukua miili ya wafu na kuivesha nguo mpya, kisha kuifanyia sherehe.

Licha ya mila hiyo, watu wa kabila la Toraja wana utamaduni ambao unashangaza kidogo kwa huku kwetu, huenda wao wanaona ni kawaida lakini kwa Afrika na dunia ni kitu cha ajabu.

Utamaduni huo ni kwamba mtoto mdogo ambaye bado hajaota meno akifariki, huwa hazikwi ardhini kama watu wengi wanavyozika duniani, bali wao huwa tofauti, mama wa mtoto humchukua mtoto na kumviriga kwenye nguo maalum, na kisha kwenda msituni, msituni huko kuna miti ambayo imetengewa maalum kwa ajili ya kuwazika watoto hao.

Mama akishafika msituni huchimba tundu kubwa kwenye mti na kumtumbukiza mtoto huyo, kisha kulifunga. Mti unapoendelea kukua na kujiziba lile tundu, huamini mtoto huyo amechukuliwa na mti huo kama asili ya dunia. (nature).

Huo ndio utaratibu wao kwa watoto wote wanaozaliwa kwenye jamii hiyo ya Kiindonesia, inayopatikana huko Tana kusini mwa Saluwesi.