Ijumaa , 27th Mar , 2020

Afisa Habari wa Simba, Haji Manara amezungumzia kuhusu kitendo chake cha kuhudhuria mazishi kabla ya siku 14 za kujitenga kutokana na tishio la virusi vya Corona.

Haji Manara

Jana Machi 26, 2020, Manara alihudhuria mazishi ya aliyekuwa Msemaji wa klabu hiyo,  Asha Haji aliyefariki Machi 25 katika hospitali ya Hindu Mandal Jijini Dar es Salaam, ambapo alitokea katika Karantini yake ambayo aliiandaa mwenyewe kwa siku 14 baada ya kurejea nchini akitokea katika ziara yake barani Ulaya.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Manara amesema kuwa yeye hana maambukizi ya virusi vya Corona baada ya kupima mara mbili hapa nchini na aliamua kujiweka Karantini kwa hiyari yake, hivyo hajakatazwa kuhudhuria shughuli yoyote.

"Wapo watu wananilaumu eti kwanini nimeenda msibani wakati nipo katika Karantini?. Niwafahamishe ni mimi binafsi kwa hiyari yangu niliamua kukaa Karantini baada ya kutoka safari bila kushurutishwa na yoyote!", amesema Manara.

"Agizo la Mh Rais la kuwataka wote wanaorejea kutoka nje kukaa Karantini kwa siku 14, limetolewa mimi nikiwa tayari nimesharejea, nilipimwa mara mbili hapa nchini na kubainika nipo salama lakini nikasema ngoja nikae mwenyewe kidogo kujisikilizia. Sasa kwa msiba wa dada yangu na kwa kuwa nipo salama baada ya vipimo vya kitabibu kuonyesha hivyo, sikuweza kukaa ndani tena", ameongeza.

Manara pia amesema kuwa watu wanaomlaumu ni wale ambao wanamuombea mabaya ili asifanikiwe.