Alhamisi , 1st Aug , 2019

Mbunge wa Hanang Mh Mary Nagu, ameipongeza East Africa Television na East Africa Radio kupitia kampeni ya Namthamini na kudai kuwa tangu ameshiriki kwenye mwaka wa kwanza amekuwa akiona mafanikio ya kampeni hiyo.

Timu ya Namthamini ikiwa na Mbunge wa Hanang Mary Nagu (katikati) ofisini kwake Hanang.

Akiongea ofisi kwake mbele ya timu ya Namthamini ambayo ilikuwa wilayani humo kwaajili ya kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule za Sumaye na Simbay, Nagu amesema anajivunia kampeni ya Namthamini kwani inatengeneza viongozi wanawake wa baadaye.

''Nakumbuka nilishiriki kwenye awamu ya kwanza, na tangu hapo nimekuwa nikifuatilia mnavyoendelea kuwathamini wasichana wetu shuleni kiukweli ni jambo la kupongezwa na msiache endeeleni hivyo hivyo na sisi tutawaunga mkkono kadri tunavyoweza'', amesema.

Kampeni ya Namthamini kwa mwaka 2019, imefanikisha wanafunzi wa kike zaidi ya 300, kupata taulo za kike kwa mwaka mzima ndani ya  Wilaya ya Hanang.

Wanafunzi hao wanatoka katika shule ya sekondari Simbay ambayo ni ya kutwa pamoja na shule ya sekondari Sumaye ambayo ni ya kutwa na bweni. Wasichana takribani 70 wanaotoka mbali wanakaa bweni.