Mjamzito anavyomsababishia ugonjwa wa akili mtoto

Ijumaa , 14th Sep , 2018

Dkt. Ruchius Philbert ambaye ni Afisa Muuguzi kutoka hospitali ya Taifa ya Muhimbili, mtafiti pia mkufunzi wa masuala ya afya ya akili, amesema katika sababu zinazochangia matatizo ya afya ya akili, mama mjamzito ni kisababishi kikuu kwa mtoto aliye tumboni.

Mwanamke mwenye ujauzito

Akizungumza katika kipindi cha SUPAMIX cha East Africa Radio leo, Philbert amesema mama mjamzito asipofuata kanuni za ulaji kwa wakati ikiwemo lishe duni, ni sababu kuu kupelekea mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo ya akili au kumpata baadaye ukubwani.

''Tafiti mbalimbali zimefanyika na kuonesha hakuna chanzo kimoja cha ugonjwa wa akili, lakini lishe duni kwa mama mjamzito ni sababu pekee kubwa kupelekea mtoto azaliwe na tatizo la afya ya akili, kwani malezi ya mtoto huanzia tumboni mwa mama, na matokeo yake ni mtoto kuwa na utindio wa ubongo'', ameeleza Dkt. Philbert.

Aidha, Dkt. Philbert amezitaja sababu kuu tatu ambazo husababisha mvurugikano wa afya ya akili, ambazo ni za kibailojia ikiwa ni njia ya kurithishana 'vina saba' kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, nyingine ni kisakolojia hutokea kama mtu ananyanyapaliwa au kutengwa, na sababu ya tatu ni ya kijamii ambayo uhusisha mazoea ya jamii inayomzunguka mtu, mfano unywaji wa vilevi kupita kiasi ikiwemo bangi, pombe na mifarakano ya kwenye jamii.

Dkt. ameendelea kwa kusema ''dalili za awali za ugonjwa wa akili hazigunduliki kwa haraka sana, ndio maana watu wengi hukumbwa na tatizo hili, hivyo basi sisi kama wataalam tunashauri mtu  kuonana na wataalam
wa masuala ya akili mara kwa mara kwa ajili ya ushauri tiba''.

Kila mwaka tarehe 10, Oktoba hufanyika maadhimisho ya Afya ya Akili duniani kote, mwaka jana 2017 nchini Tanzania katika maadhimisho hayo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alitoa takwimu kutoka Shirika la Afya duniani (WHO)zinaonyesha mmoja kati ya watu wanne alishapata au alishaona mtu mwenye matatizo ya kiakili.