Mmiliki wa Facebook atuma ombi kwa serikali

Jumatatu , 1st Apr , 2019

Mmiliki wa Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Mark Zuckerberg amezitaka serikali kote ulimwenguni kusaidia kuweka sheria za udhibiti wa taarifa za intaneti.

Picha ya nembo ya Facebook.

Zuckerberg ameandika barua ya wazi akitoa wito sheria ziwekwe ili kufuatilia taarifa za intaneti. Katika waraka wake wa wazi uliochapishwa na gazeti la Washington Post anasema jukumu la ufuatiliaji wa maudhui hatari ni kubwa sana kwa kampuni ya Facebook.

Zuckerberg ameongeza kuwa Facebook inabuni bodi huru ili watu waweze kukata rufaa juu ya uamuzi mbalimbali juu ya kile kinachotumwa na kile kinachoondolewa kwenye mtandao huo.

Anasema ziwepo sheria za pamoja ambazo mitandao yote ya habari ya kijamii inahitaji kufuata, kudhibiti kutekelezwa na kampuni nyingine, kudhibiti kusambaa kwa taarifa za zinazosababisha madhara.

Pia, ameshauri kampuni zote za teknolojia kutoa ripoti ya wazi kila baada ya miezi mitatu, sawia na ripoti yao ya fedha. Ameshauri sheria kali ziwekwe kote duniani kulinda maadili ya uchaguzi na kuwapo kwa viwango sawa kwa tovuti zote za kuwatambua wanasiasa.

Wito wa mmiliki huyo wa Facebook unakuja wiki mbili baada ya mtu mwenye silaha kutumia mtandao huo kusambaza video yake moja alipokuwa akiushambulia msikiti eneo la Christchurch, New Zealand.